Friday, February 19, 2016

 
TAMKO LA HAKIELIMU JUU YA BAJETI YA ELIMU MWAKA WA FEDHA 2015/2016

UTANGULIZI
Mwaka wa fedha 2015/2016 unatazamiwa kuwa wa changamoto nyingi katika ukusanyaji na ugawaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi na utoaji huduma. Ni mwaka wa matukio makubwa; Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015, kura ya maoni na mchakato wa upatikanaji katiba mpya, utekelezaji wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na uzibaji wa mapengo ya kifedha yaliyotokana na wahisani kupunguza misaada kufuatia kashfa za rushwa kama ile ya ESCROW. Hizi ni sehemu tu ya changamoto ambazo bajeti inayotarajiwa itapaswa kushughulikia.

Wakati sura ya changamoto hizi ni ya jumla, athari za kutoshugulikiwa kwake kwa umakini zitasambaa katika sekta moja moja na kuathiri utoaji huduma kwa jamii; sekta ya elimu ikiwa moja wapo. Ndiyo maana, ni muhimu zaidi mwaka huu kuliko miaka mingine kwa serikali kushauriwa kwa ufasaha kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kama itaendelea kupanga bajeti yake kwa mazoea.

HakiElimu inatambua juhudi kubwa ambazo zimefanywa na zinaendelea kufanywa na serikali katika kuboresha elimu nchini. Kupatikana kwa Sera mpya ya Elimu ya mwaka 2014, kuwepo kwa mipango inayoonesha nia ya dhati ya kupata matokeo mazuri katika utoaji huduma kama BRN, na kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya elimu katika upangaji bajeti ni mfano wa juhudi hizo. Tunaipongeza sana serikali kwa juhudi hizi.

Hata hivyo, yako mapungufu mengi katika utekelezaji ambayo yanapoteza kabisa uzito wa juhudi hizo. Bila kuchukua hatua stahiki, iko hatari ya mwaka ujao wa fedha kuwa mgumu zaidi kiutendaji. Hivyo, wakati serikali ikipanga juu ya ukusanyaji na ugawaji wa rasilimali fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 ni muhimu kuzingatia sana maeneo tunayoyaainisha katika tamko hili.

Hoja za kisera
Tunaipongeza serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014. Matumaini yetu ni kuwa serikali itaharakisha utungwaji au urekebishaji wa sheria ya elimu ili sera hii ianze kutumika mara moja. Hata hivyo yako mambo ambayo HakiElimu tunaona yanaweza kurudisha au kukwamisha utekelezaji wa sera hii mpya ambayo kimsingi yanahitaji suluhisho la kibajeti.

Mpango wa utoaji elimu bure: Sera mpya ya Elimu 2014 inasema “Serikali itahakikisha kuwa elimu msingi katika mfumo wa umma inatolewa bila ada.” Wakati tunaamini kuwa huu mpango ni mzuri ambao utaleta nafuu hasa kwa watanzania masikini mijini na vijijini, ni muhimu pia kujiuliza kama ni mpango unaotekelezeka?  Tunafahamu jinsi serikali imekuwa ikitekeleza bajeti pungufu kila mwaka katika utoaji huduma kama elimu, maji na afya.

Katika uwasilishaji wa makadirio ya mapato na matumizi katika mpango wa bajeti 2015/16 serikali inapaswa iainishe  ni jinsi gani imejipanga kuhakikisha tamko hili la utoaji elimu bila ada litatekelezeka.  Ni muhimu kwa serikali kufafanua hili katika bajeti hii kwa kuwa tayari tamko hili limeanza kuleta mvutano kati ya wazazi na walezi na watekelezaji wa sera na mipango kama vile wakuu wa shule na waratibu. Baadhi ya wanajamii wamerudi nyuma katika uchangiaji wa elimu kwa sababu ya tamko hili la kisera.

Serikali ifafanue ni kwa jinsi gani elimu msingi inaweza kutolewa bila ada wakati inakabiliwa na changamoto lukuki zitokanazo na uhaba wa fedha hata katika kipindi hiki ambacho ada zinaondolewa. Bajeti iainishe ni chanzo gani cha mapato kinakwenda kuziba pengo litakalo- achwa na kutotozwa kwa ada za masomo.

Kiwango cha ruzuku katika sera mpya; Ufadhili wa elimu ya msingi na sekondari wakati wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1995 ulifanyika kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Serikali iliazimia kutoa ruzuku kwa shule sawa na shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi shule ya msingi na shilingi 25,000 kwa mwanafunzi sekondari.

Je, utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu 2014 utaendelea kufanyika kupitia mipango ya MMEM na MMES?  Ikiwa jibu ni HAPANA, serikali iseme wazi katika mpango wa bajeti ya 2015/16 ni vipi utekelezaji wa sera mpya utafanyika. Kama jibu ni NDIYO, basi iseme ni kiasi gani kwa kila mwanafunzi wa msingi na wa sekondari kitatolewa?  Ni vema kukumbuka pia kuwa viwango vya 10,000 na 25,000 vimepangwa tangu miaka ya 2002 na 2004, miaka zaidi ya kumi nyuma.

Gharama za maisha zimepanda, mfumuko wa bei umeongezeka na sarafu ya Tanzania imeendelea kushuka thamani. Utakuwa ni uigizaji kama serikali itang’ang’ania kuendelea kutumia viwango vile vile vya ruzuku shuleni wakati uwezo wake wa kununua umepungua. Ni rai yetu kuwa, serikali itamke katika mpago wake wa bajeti 2015/16 ni jinsi gani itarekebisha viwango hivi ili viendane na gharama halisi za maisha badala ya kupanga kwa mazoea.

Sera mpya na changamoto za bajeti ya ruzuku: Ufanisi wa utekelezaji wa azma ya MMEM na MMES juu ya utoaji ruzuku umekuwa wa chini sana katika miaka kumi iliyopita. Changamoto kubwa zimekuwa kiwango cha chini zaidi ya kilichokusudiwa na uchelewaji wa ruzuku shuleni. Hata hiyo, sera mpya imeongeza changamoto nyingine ya kufutwa kwa ada shuleni.

Hali ya upelekaji ruzuku shuleni haijawahi kuwa ya kuridhisha tangu kuanza kwa program za MMEM na MMES. Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa inaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2013/2014 serikali iliweza kutoa sh 4,200 badala ya sh 10,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi kwa shule za msingi na pia kutoa sh 12,000 badala y ash 25,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi kwa shule za sekondari.

Matarajio ya umma katika Sera mpya ya Elimu 2014 yalikuwa ni kupatiwa ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali ikiwamo ya utoaji usioridhisha wa ruzuku shuleni. Kwa bahati mbaya sera hii haisemi chochote kuhusu mpango wa kuhakikisha shule zinapata ruzuku iliyokusudiwa kwa wakati na kamilifu. Badala yake, sera hii inataja kufuta ada ya masomo na hivyo kuzidi kupunguza vyanzo vya mapato shuleni;  hii ni changamoto nyingine.

Bajeti ya mwaka huu ni lazima ije na sura ya ufumbuzi wa mwanya huu wa kisera, iwe na maelezo ya kifedha yanayofafanua jinsi ya kuziba pengo la uhaba wa ruzuku, uchelewaji na kufutwa kwa ada shuleni. Serikali itambue hofu ya wananchi ni kuwa kufutwa kwa ada shuleni kutawaongezea wao mzigo wa uendeshaji shule, au kutaua shule za umma na hivyo kuwalazimisha wazazi kulipia shule binafsi ambazo ni ghali sana.

Uwezo wa Serikali katika ukusanyaji kodi: Katika gazeti la “The Citizen” Februari 2, 2015, Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya alinukuliwa akikiri bungeni kuwa serikali imekuwa ikijiendesha kwa kutegemea makusanyo kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) pekee tangu Julai 2014. Lakini kwa mujibu wa kumbukumbu za TRA, mamlaka hii ina uwezo wa kukusanya shilingi bilioni 800 tu kwa mwezi. Mpaka Mwaka 2013, wastani wa bajeti ya mishahara ya watumishi wa umma pekee kwa mwezi ulikuwa Tshs. Bilioni 403, takribani nusu ya makusanyo yote ya TRA kwa mwezi. Kwa mwenendo huu serikali inapata wapi fedha kwa ajili ya kuwekeza katika miradi na kutoa huduma kwa wananchi wake?

Hali hii ya kutegemea chanzo kimoja tu cha mapato imechagizwa na hatua za hivi karibuni za wafadhili kusitisha ufadhili wao katika mfuko wa pamoja wa bajeti (GBS) wa kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 1,000 kutokana na kashfa za ufisadi ikiwamo ya ESCROW. Ingawa tayari baadhi ya wafadhili wameamua kulegeza masharti yao lakini bado uchangiaji wa GBS ni wa kusuasua na usio wa kutegemewa kama serikali yenyewe inavyokiri kupitia mwongozo wa makadirio ya bajeti wa mwaka 2015/16.

Ufadhili wa wahisani kupitia GBS; serikali inaeleza katika mwongozo wa bajeti kuwa ufadhili wa bajeti ya taifa utatokana na vyanzo vikuu vitatu; kodi na tozo shilingi bilioni 14,684, mikopo ya ndani na nje shilingi bilioni 4,220.1 na ufadhili wa wahisani katika mfuko wa pamoja wa bajeti (GBS) kiasi kisichofahamika.

Serikali inasema, kutokana na mwenendo usioeleweka wa wahisani katika kuchangia mfuko wa pamoja wa bajeti, imeamua katika makadirio ya bajeti ya mwaka 2015/16 kutoainisha ni kiasi gani kinatarajiwa kuchangiwa na wahisani katika mfuko huu na kuwa kiwango kilichochangiwa kitatambuliwa baada ya wahisani kutoa kiasi hicho.

Hii ina maana kuwa kiasi cha GBS kitatambuliwa baada ya makadirio ya mwaka huu kuidhinishwa na bunge na utekelezaji kuwa umeanza. Athari za aina hii ya upangaji wa Bajeti ni kubwa na ziko wazi. Kwanza, inafanya upangaji bajeti kwa idara, taasisi na wizara kuwa mgumu kwa kuwa hawajui ni kiasi gani hasa serikali itatumia kwa mwaka husika wa fedha. Pili, hata kiasi hicho kikiletwa kinaweza kutumika kwa matumizi yasiyo halali kwa kuwa hakikuidhinishwa na Bunge na huu unaweza kuwa mwanya wa rushwa na ufisadi. Kuelekea bajeti tunawataka wabunge na kamati kuliangalia hili ili kabla ya kuidhinishwa kwa bajeti liweze kutolewa ufafanuzi.

Kuendelea kukua kwa Deni la Taifa: Miongoni mwa mizigo ambayo wananchi wanabebeshwa ni huu wa deni la taifa. Sehemu kubwa ya makusanyo ya kodi kutoka TRA huishia kulipia deni la taifa na kulipa mishahara ya watumishi wa umma hivyo kuyaacha maeneo mengine kama uwekezaji katika elimu yakiwa na upungufu wa fedha.

Kwa mujibu wa mwongozo wa bajeti ya 2015/16, Deni la Taifa limefikia kiasi cha bilioni 30,892.8 hadi mwisho wa mwezi Juni 2014. Kiwango hiki ni sawa na asilimia 55 ya pato la taifa kwa mwaka yaani GDP au sawa na bajeti ya Taifa  kwa miaka miwili mfululizo. Kasi ya ongezeko la Deni la Taifa ni ya kutisha, hadi mwisho wa mwaka 2013 deni la taifa lilikuwa shilingi billion 25,008.3. Hii ina maana kuwa ndani ya mwaka mmoja zaidi ya bilioni 5,884.5 zimeongezeka sawa na ongezeko la takribani asilimia 23.5% kwa mwaka.

Ongezeko la bilioni 5,884.5 ni kubwa mno. Mathalani mwaka wa fedha 2014/15 jumla ya bajeti ya sekta nzima ya elimu kwa mwaka ilikuwa shilingi bilioni 3,465, kikiwa ni kiwango kidogo zaidi ya kiwango cha ongezeko la deni la taifa kwa mwaka huo. Kama mwenendo huu usipodhibitiwa ni wazi kuwa baada ya muda mfupi serikali itakuwa na deni kubwa lisilolipika ambapo madhara yake katika uchumi na utoaji huduma za jamii ni makubwa pia. Bunge ni lazima liisimamie serikali ili kupunguza kasi hii ya ukuaji wa deni la taifa na kuendelea kulipa ili kuepukana na kuwa taifaombaomba.

Ukweli juu ya madai ya walimu: Chama cha Walimu nchini (CWT) kupitia raisi wake Gratian Mukoba, kimetangaza nia ya kususia upigaji kura ya maoni juu ya Katiba Mpya mpaka serikali itakapokamilisha kulipa madai yao yafikiayo shilingi billion 16 mpaka sasa. Wakati huo huo taarifa za ripoti ya BRN ukurasa wa 28 unataja kuwa deni ambalo limehakikiwa na ambalo serikali inapaswa kuwalipa waalimu ni shilingi bilioni 5.7 tu, huku Katibu Mkuu wizara ya elimu Suifuni Mchome akikiri kutambua deni lililobaki kuwa ni bilioni 16 kama inavyodaiwa na CWT.

Mvutano huu unazidi kuwashusha moyo wa kufanya kazi walimu. Taarifa za utafiti zinaonesha ni 27 -39% tu ya walimu wanafurahia kufanya kazi yao na wanajituma, huku 61% ya walimu hawaridhiki na hawajitumi katika maeneo yao ya kazi. Ni kwa namna gani tunatarajia ufanisi katika elimu?

Ni muhimu kuondoa hizi sintofahamu na kuweka taarifa sahihi kuhusu madai ya walimu, na pia kulipa kabisa kiasi kilichobaki ili kusiwe na visingizio vya walimu kutofundisha au kujituma kazini. Ni muhimu katika bajeti ya mwaka huu 2015 /16 serikali ikajipanga kumaliza mvutano huu na walimu kwa kupanga bajeti ya kulipa malimbikizo yao. Aidha, ni muhimu kuweka utaratibu ambao utadhibiti kuongezeka kiholela kwa deni hili tena.

Ufanisi BRN na ukaguzi wa shule zetu: Ripoti ya kwanza ya mwaka ya utekelezaji wa Mpango wa matokeo makubwa sasa, (BRN) imetoka mwezi Februari 2015. Katika ripoti hiyo sekta ya elimu inaonekana kuongoza kwa kufikia malengo kwa 81%. Malengo ambayo yanatajwa kufikiwa ni pamoja na kufanikisha uandaaji wa wiki ya kwanza ya elimu,  kuwatambua na kuwatunuku watoto 3,044 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kwa mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne, kupanga na kuzichapisha shule kulingana na ufaulu, na kufanikisha upatikanaji wa taarifa za elimu kwa umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Tunaamini kuwa falsafa nyuma ya BRN ni nzuri na inayofaa kukumbatiwa, lakini methodolojia ya utekelezaji wake imetazama maeneo ambayo si changamoto za msingi katika sekta ya elimu. Utaratibu wa kutunuku zawadi, kupanga shule kwa madaraja na uandaaji wa sherehe kuadhimisha siku fulani umekuwepo kwa muda mrefu, hivyo hatudhani kama yalipaswa kuwa maeneo ya kutiliwa mkazo na BRN.

BRN unatajwa kuwa utaratibu wa kuchochea mabadiriko katika utendaji. Ni vema mpango huu ungejikita katika kusimamia upelekaji wa ruzuku na ukaguzi shuleni ambao ndio ungesaidia kugundua mapungufu ya kiutendaji na kupendekeza njia za utatuzi. Wakati BRN ikitumia pesa nyingi kuandaa sherehe, bajeti ya ukaguzi shuleni imeendelea kuporiomoka mwaka hadi mwaka. Wastani wa ufanisi katika lengo la ukaguzi umebaki kuwa 42.5% kwa shule za msingi na 43.3% kwa sekondari na vyuo vya ualimu.

Ili kuimarisha utawala na utendaji mashuleni ni muhimu taasisi hizi zikafanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara. Ni lazima watendaji wasijisahau na shughuli nyingine za maisha. Bunge lihakikishe kuwa katika bajeti ya 2015/16, linaishauri serikali kuangalia upya jinsi ya utekelezaji wa BRN katika kutatua changamoto za msingi kama ukaguzi na kurudisha morali ya kufundisha na kujifunza.

Hitimisho
Sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto nyingi za kisera na kiutendaji. Miongoni mwa maeneo yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka ni pamoja na hayo yaliyoainishwa hapo juu na suala la kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Utekelezaji wa utaratibu wa ugatuaji madaraka mathalani, umeifanya sekta ya elimu kutekelezwa na wizara zaidi ya moja.Matiokeo yake kumekuwa  na changamoto za muingiliano wa baadhi ya majukumu katika utekelezaji wa ugatuaji kwa upande wa utendaji na usimamiaji wa elimu kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na OWM-TAMISEMI unaorudisha nyuma ufanisi katika utoaji elimu bora na yenye usawa. Umefika wakati sasa serikali iweke utaratibu wa utekelezaji elimu wazi. Ifahamimike ni wapi hasa malalamiko juu ya ubora wa elimu na usawa yanapaswa kupelekwa na kushughulikiwa, vinginevyo utoaji elimu utaendelea kupigwa danadana bila kujua hasa mamlaka inayopaswa kuwajibika ni ipi.

Ni wakati muafaka kwa ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG), kupitia hesabu za sekta ya elimu. Ukaguzi maalumu unapaswa ufanyike kupima ufanisi wa program za MMEM na MMES, BRN na mingine ambayo imekuwa ikitumika kufadhili elimu. Uchunguzi huu wa kitafiti utasaidia kuishauri serikali iwapo inaelekea mahali sahihi au kuna haja ya kuangalia upya mbinu na utaratibu wa ufadhili katika sekta ya elimu.

Godfrey Boniventura
Kaimu Mkurugenzi

No comments:

Post a Comment