Thursday, October 30, 2014

ELIMU YA TANZANIA SASA NI MZIGO USIOBEBEKA



Suala la kuporomoka kwa ubora wa elimu ya Tanzania na mfumo wake wa uendeshaji ni moja ya mambo yanayoendelea kutawala mazungumzo ya watanzania kwa sasa.

Kwa walio wengi, suala hili halina kificho tena kutokana na ushahidi mbalimbali, kama vile utata wa matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kuhitimu masomo ya msingi na yale ya sekondari.

Tukichukulia kwa mfano, matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana, kati ya watahaniwa 431,650 waliofanya mtihani, watahaniwa waliofaulu kwa ubora , yaani daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 35,599 tu, sawa na asilimia nane.

Hii inamaanisha kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya watahaniwa hawakuwa na ufaulu wenye kiwango bora.

Ushahidi mwingine ni ule wa wanafunzi kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kama ilivyoripotiwa katika baadhi ya mikoa ya Lindi, Dodoma na Shinyanga.

Kwamba mwanafunzi amesoma mwaka moja elimu ya ngazi ya chekechea na miaka saba elimu ya shule ya msingi, lakini hajui kusoma wala kuandika ni suala linalostajaabisha.

Lakini lingine lililoonyesha kuwepo kwa tatizo la kuporomoka kwa ubora wa elimu inayotolewa katika shule zetu, ni tafiti mbalimbali.

Shirika lisilo la kiserikali la Uwezo kwa mfano, ambalo limekuwa likitoa tafiti za ubora wa elimu katika nchi za Afrika Mashariki, yaani za Tanzania, Uganda na Kenya, limeonyesha namna Tanzania inavyozidi kuachwa nyuma kielimu.

Katika utafiti wake wa mwaka 2011 uliojumuisha nchi zote tatu, Uwezo liligundua kuwa wengi wa wanafunzi wa darasa la tatu ambao walipaswa kuwa na stadi za hesabu na kusoma kwa ngazi ya darasa la pili, hawakuwa nayo kwa nchi zote.

Utafiti ulibainisha kwa ulinganifu kwa nchi zote tatu, karibu wanafunzi wote wa darasa la saba kwa Uganda na Kenya, waliweza kufaulu majaribio yote ya ngazi ya darasa la pili waliyopewa.

Hali ilikuwa tofauti kwa Tanzania, kwani ni asilimia 50 hadi 80 ya wanafunzi wa darasa la saba, ndiyo waliweza kufaulu majaribio ya ngazi hiyo

Mifano hiyo mitatu inahalalisha sababu za kushuka kwa ubora wa elimu, kutawala sana katika mazungumzo ya watanzania na wadau wa elimu ya Tanzania, ikiwamo Benki ya Dunia (WB)

Serikali na wadau wa elimu hadi sasa hawajaweka bayana sababu za kuporomoka kwa ubora wa elimu kiutafiti.

Serikali nayo imekiri kushuka kwa ubora wa elimu inayotolewa na shule zake kupitia kwenye hotuba ya Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa aliyoitoa Agosti Mwaka huu.

Dk. Kawambwa alikiri uwepo wa tatizo hilo wakati wa uzinduzi wa Utekelezaji wa mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu, uliofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Dk Kawambwa katika kutekeleza mpango huo wa serikali kwa sekta ya elimu, wizara yake iliwakusanya washiriki 34 kutoka taasisi 31 zikiwamo za serikali na zisizo za serikali, kwa lengo la kutafakari kwa kina changamoto zinazoathiri sekta hiyo.

“Changamoto kubwa iliyoanishwa na washiriki ni utambuzi kwamba, ingawa shule zimeongezeka na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi vimeongezeka, ubora wa elimu unashuka, hususan kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu katika elimu ya msingi na sekondari,” kwa mujibu wa Dk Kawambwa.

Kwamba waziri hakueleza dhahiri sababu ya kushuka kwa ubora wa elimu, na badala yake anaeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kuathiri utoaji wa elimu bora, inathibitisha ukubwa wa tatizo.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu, uwezo mdogo wa walimu kufundisha, motisha kwa walimu, uwajibikaji wa walimu na watumishi wa sekta ya elimu.

Changamoto nyingine ni zile za upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, miundo mbinu isiyokidhi mahitaji, mapungufu katika usimamizi wa elimu ngazi ya shule, ufutiliaji na tathmini na uthibiti wa ubora wa shule.

Kilichonisukuma kuandika makala hii,ni  kutokana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) katika shule mbalimbali, kuangalia sababu za kushuka kwa ubora wa elimu nchini, mwaka 2010.

Matokeo ya utafiti huo ambao uliweka bayana moja ya sababu za kushuka kwa ubora wa elimu nchini, ulifafanuliwa na Mtaalamu  Kiongozi wa benki hiyo, upande wa Elimu wa Maendeleo ya Rasilimali Watu,Kanda ya Afrika, Arun Joshi.

Ilikuwa ni kwenye mazungumzo maalumu aliyoyafanya Joshi na gazeti la Nipashe, wakati wa hafla iliongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Rasiliamali Watu wa WB, kanda ya Afrika, Ritva Reinikka.

Hafla hiyo ilitumiwa na WB kutangaza kutenga kiasi cha shilingi bilioni 162 kwa miaka minne kuanzia 2014 hadi 2018 kwa ajili ya kuchagiza mpango wa serikali wa BRN, kwa upande wa sekta ya elimu.

Akizungumzia utafiti huo,Joshi alisema uligundua kuwa walimu wanatumia muda kidogo sana wa kufanya kazi ya kufundisha.

“Utafiti wetu uligundua walimu wanatumia muda wa wastani wa saa mbili na dakika nne tu za kufundisha, tofauti na saa tano zinazotakiwa kwa kutwa nzima,” kwa mujibu wa Joshi.

Anasema kwa shule zilizo mjini, hali ni mbaya zaidi, kwani huko walimu wanatumia saa moja na ushee, ukilinganisha na wale wa shule zilizo vijijini.

Josh anasema utafiti umegundua kuwa saa nyingi zinatumiwa na walimu kufanya shughuli zingine zisizokuwa na uhusiano na taaluma wakati wa kazi, wakati mwingine wakiishia kupiga soga, kiashirio kimojawapo cha kutokuwa na morali wa kufundisha.

“Hapa ndipo penye tatizo la msingi kwa sababu ikiwa walimu hawafundishi kwa mujibu wa muda unaotakiwa, huwezi ukatarajia ubora ukaongezeka ila ni yumkini kwamba utashuka tu,” anasema.

Anasema hali hiyo ndiyo iliyosababisha waone umuhimu wa kuchagiza jitihada  za serikali, kwa kutoa fedha zitakazotumika kugharamia pamoja na mambo mengine, mafunzo zaidi ya walimu wa shule za msingi pamoja na kuwamotisha ili wafundishe kwa muda wote unaotakiwa.

Ni muda mrefu sasa wadau wamekuwa wakitaja sababu ya walimu kukosa morali wa kufundisha kuwa ndiyo sababu ya msingi, ya kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini.

Kukosekana huku kwa morali kama utafiti wa WB ulivyobainisha, mbali na mambo mengine, unatokana na kukosekana kwa motisha kwa walimu.

Pamoja na udogo wa mishahara, walimu wamekuwa wanadai malimbikizo ya mishahara, posho na malipo mengine bila mafanikio.

Wakati serikali, kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ikiwa katika utekelezaji wa mikakati ya BRN, ni muhimu ikatibu kwanza suala la morali kwa walimu.

Nia ni kuwawezesha wafundishe kwa muda unaotakiwa wa kufanyakazi kwa mujibu wa miongozo, ili kuboresha kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kitanzania, na hatimaye taifa liwe na wahitimu wenye stadi stahiki kwa ustawi wa nchi.