a shule ya sekondari ya wasichana wenye vipaji ya Kilakala wakifurahia jambo wakati wa mahafali.
TUNAPOUANZA mwaka 2016, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa miongoni mwa majukumu yake mbalimbali, imejipanga kikamilifu
kusimamia utekelezaji wa dhana ya elimu bila malipo.
Dhana hii inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya
aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi/walezi wa wanafunzi kama
ilivyoainishwa katika ibara ya 3.1.5 ya Sera ya Elimu na Mafunzo (2014)
na ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya
mwaka 2015.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Waziri wa
Nchi, George Simbachawene anabainisha kuwa Serikali imejipanga
kugharamia uendeshaji wa shule ili kuziba pengo la ada na michango
mbalimbali iliyokuwa inatolewa na wazazi na walezi. Anaeleza kuwa kwa
kuanzia Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 131.4 ikiwa ni fedha za
ruzuku ya uendeshaji wa shule, chakula, mitihani na fidia ya ada.
Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja shuleni kutoka Hazina kwa
wastani wa Sh bilioni 18.777 kila mwezi kwa ajili ya: Ruzuku ya
Uendeshaji wa Shule (Capitation Grants- CG) ya Sh 10,000 kwa mwanafunzi
wa shule za msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.
Pia akaunti hiyo itapokea fedha za wanafunzi wa bweni ambapo Serikali
itatoa Sh 1,500 kwa siku kwa mwanafunzi wa bweni wa shule za msingi na
sekondari kwa ajili ya chakula; fidia ada ya Sh 20,000 kwa mwanafunzi wa
kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa bweni wa kidato cha kwanza hadi
cha nne kwa mwaka.
Mzazi hatatakiwa kulipa fedha za mitihani wala michango yoyote hivyo
wazazi wanahimishwa kuwapeleka shule watoto wao ili waweze kupata elimu
itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha. Anafafanua kuwa upo
umuhimu wa kutoa elimu msingi bila malipo kwani kufanya hivyo
kutaongeza kiwango cha uandikishaji kwa watoto wote wenye rika lengwa,
kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi na pia ufaulu wa wanafunzi katika
mitihani mbalimbali utaongezeka.
Simbachawene anasema kuwa katika utekelezaji wa uendeshaji wa elimu
msingi bila malipo imeainisha majukumu ya serikali kuhusu utoaji wa
elimumsingi bila malipo kama yalivyoelezwa katika Waraka wa Elimu Namba
sita wa mwaka 2015. “Majukumu hayo ni pamoja na kutafasiri sera kwa
kutoa nyaraka, miongozo na kusimamia utekelezaji wake katika ngazi
mbalimbali za kiutawala kuanzia wizara, mikoa, wilaya, halmashauri, kata
na shule,” anaeleza Simbachawene.
Mikakati mingine iliyowekwa na Ofisi ya Rais, Tamisemi, katika mwaka
2016 ni kuhakikisha kuwa tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi
shuleni linamalizika katika kipindi kijacho cha miezi sita. Simbachawene
anasema hakuna sababu ya kukosekana kwa madawati shuleni, kwani, nchi
ina misitu ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza mbao na madawati, hivyo
amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kushirikiana na Watendaji wa
Halmashauri kuhakikisha tatizo hilo linamalizwa.
“Tunawaahidi Watanzania kuwa ndani ya miezi sita hakuna mtoto
atakayekaa chini kwa kukosa madawati, nami sitakubali nikae mwaka mmoja
na kushuhudia watoto wetu wanaaendelea kukaa chini kwa kukosa madawati,”
Simbachawene. Waziri Simbachawene anayabainisha majukumu ya Ofisi ya
Rais Tamisemi kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mabadiliko
wanayoyatarajia wananchi kutoka kwa serikali yao yanatekelezwa na hivyo
anatoa wito kwa watumishi wa ofisi yake kuchapa kazi kuendana na kasi ya
viongozi wao.
Anaeleza kuwa Watanzania wana matarajio makubwa na Serikali ya awamu
ya tano, na akataka Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ndizo zenye
dhamana kubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kama vile
kusimamia utekelezaji wa huduma za elimu bure kuanzia chekechea hadi
kidato cha nne na kuhakikisha kuwa zinatolewa bure. Simbachawene anasema
pamoja na utekelezaji na usimamizi wa shughuli za elimu katika Mamlaka
za Serikali za Mitaa, wajibu mwingine kwa mamlaka hizo ni kusimamia
shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kujikinga na
maradhi kama kipindupindu.
Simbachawene anazipongeza halmashauri zote kwa namna ilivyoshiriki
katika kufanikisha zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao
na hivyo kuitikia vyema mwito wa Rais Dk John Magufuli. Simbachawene
anawataka wananchi wote kuuendeleza utamaduni wa kufanya usafi mara kwa
mara na kwamba serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa inaandaa
mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu wa uzoaji taka katika
makazi ya watu.
Anasema moja ya mikakati ya muda mfupi ni kuhakikisha kuwa taka
zinazokusanywa hazikai muda mrefu katika makazi ya watu na kwamba
ameziagiza halmashauri kuhakikisha kuwa zinaandaa utaratibu maalum kwa
magari ya kuzoa taka kufanya kazi hiyo usiku. Waziri Simbachawene
anasema mpango huo utarahisisha uzoaji taka kwa wingi na kwa haraka
kwani usiku hakuna msongamano mkubwa wa magari kama ilivyo mchana na
kwamba hatua hiyo itapunguza gharama na pia kuyawezesha magari hayo
kufanya safari nyingi zaidi za kutupa taka hizo katika maeneo
yaliyotengwa.
“Ili kurahisisha zoezi hilo kila mtaa unapaswa kutenga maeneo maalum
ambayo wananchi watahifadhi taka hizo na pia kuchukuliwa kwa urahisi na
magari ya kuzoa taka,” anasema Simbachawene. Waziri Simbachawene
anaongeza kuwa ni wajibu wa kila mkazi katika familia kuhakikisha
anazihifadhi taka katika eneo lililotengwa ili kutoleta bughudha kwa
wakazi wengine.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Selemani Said Jafo, ametaka halmashauri zote nchini
ambazo bado zinaendelea kukusanya mapato yake bila ya kutumia mfumo wa
kielektroniki ziwe zimefanya hivyo kabla ya tarehe 10 Januari 2016.
Jaffo anawataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa agizo
lake linatekelezwa na kuhakikisha kuwa mfumo huo unafanyakazi katika
idara zote muhimu za halmashauri ikiwemo Utawala, Afya na Maliasili.
Anasema kuwepo kwa mfumo huo kutazisaidia halmashauri kuboresha
ukusanyaji wa mapato na hivyo kuwa na ongezeko la fedha kwa ajili ya
kutoa huduma muhimu kwa wananchi hasa kuboresha upatikanaji wa dawa
katika zahanati na vituo vya afya vya halmashauri za wilaya. Jaffo
anasema kuwa halmashauri zimekuwa zikikusanya mapato kidogo kutokana na
kutokuwa na mfumo sahihi wa ukusanyaji mapato, na hivyo kuchangia mapato
mengi kupotea mifukoni mwa watu.
Katika kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa Mamlaka za Serikali
za Mitaa Naibu Waziri anazungumzia kero inayowakabili watumishi wa
chini katika mamlaka hizo ambao hawapati mrejesho pindi wanapohitaji
huduma mbalimbali katika halmashauri zao.
Anasema kumekuwa na mtindo kwa wakuu wa idara na Maofisa wa
Halmashauri kutoshughulikia malalamiko ya watumishi wa chini hasa madai
ya likizo za watumishi na kutopandishwa vyeo katika madaraja mbalimbali,
hivyo anawaasa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Maofisa
Utumishi kuhakikisha kuwa kero hiyo inashughulikiwa mapema mwaka huu wa
2016.
Anasema endapo ataulizwa swali bungeni kuhusu kero na malalamiko
yanayohusu watumishi kutolipwa madai ya likizo na kutopandishwa madaraja
kwa watumishi wa ngazi za chini hapo atajua kuwa Mkurugenzi na Afisa
Utumishi wa Halmashauri husika hawawezi kutimiza majukumu kulingana na
nyadhfa walizopewa. “Unakuta mtumishi anafuatilia madai yake muda mrefu
bila kupewa mrejesho, na hivyo kukosa muda wa kuendelea na majukumu yake
katika kituo cha kazi.
Anasema vijiji vingi nchini tangu vifanye uchaguzi wa Serikali za
Mitaa takribani mwaka mmoja uliopita havijafanya mikutano yake na
matokeo yake wananchi wanachangishwa fedha wala kusomewa mapato na
matumizi ya fedha hizo. “Nina taarifa kuwa vijiji vinkulishughulikia
katika mwaka 2016 ni kuhakikisha kuwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa hususani Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wanapata mafunzo ya
uongozi katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kilichopo mkoani
Dodoma".
Naibu Waziri amewapa maelekezo wakurugenzi wa halmashauri na manispaa
nchini kuandaa utaratibu wa kuwapeleka wenyeviti na mameya kupata
mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kufanyakazi kwa ufanizi zaidi.
Akizungumza mara baada ya ziara yake ya kukitembelea chuo hicho, Jafo
anasema kwa kuwa uchaguzi mkuu umepita na Madiwani wameshachaguliwa
wanatakiwa wapewe mafunzo maalumu ya muda mfupi juu ya namna ya
kusimamia na kuendesha halmashauri zao.
“Ninawaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuwasiliana na Ofisi ya
Rais, Tamisemi ili kujua namna ya kuwawezesha nauli Wenyeviti na Makamu
Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya na Manaibu Meya kuja Chuoni Hombolo
kwa siku tatu au tano kupata mafunzo juu ya uendeshaji wa Mamlaka za
Serikali za Mitaam,” anasema Jaffo. Jaffo anaeleza kuwa ni vyema mafunzo
hayo yatolewe kwa wenyeviti wa halmashauri, makamu wenyeviti, mameya na
manaibu meya ili kuwajengea uwezo kwa madiwani wate wakiwezeshwa
watakuwa na uelewa mpana wa masuala yanayohusu mikataba na malipo katika
halmashauri zao.
Anasema kuwa gharama wanazotakiwa kuwezeshwa katika halmashauri zao
ni nauli tu kwani na kusisitiza kuwa wakurugenzi hawatakiwi kuwalipa
posho Wenyeviti hao wa halmashauri kwa kuwa kila kitu kinachohusu
mafunzo hayo kitasimamiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na
Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Kwa mujibu wa ibara ya 145 na 146 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Serikali za Mitaa ni vyombo vya haki na vyenye mamlaka ya
kushiriki na kushirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli
za maendeleo na utoaji wa huduma katika sehemu zao. Ofisi ya
Rais-TAMISEMI ina wajibu wa kuzisimamia Mamlaka hizo ili ziweze
kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Mwandishi wa makala haya ni Ofisa
Habari wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment