Utafiti wa Taasisi ya Twaweza umebaini asilimia 88 ya Watanzania
wanaimani na ahadi ya elimu bure kutekelezwa katika muda uliopangwa huku
asilimia 76 wakiamini elimu hiyo kuwa na ubora zaidi.
Katika utafiti huo asilimia 15 wanaamini elimu bure haitaboresha
elimu kutokana na ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wanafunzi ambao
utatumia rasilimali nyingi.
Matokeo hayo yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye
jina la Mwanga Mpya kupitia takwimu zilizokusanywa kati ya Desemba 10,
mwaka jana na Januari 2, mwaka huu kwa upande wa Tanzania Bara.
Pamoja na wananchi kuwa na imani na ahadi ya elimu bure wengi
wamekuwa na mitazamo tofauti juu ubora wa elimu ya msingi katika kipindi
cha miaka 10 iliyopita ambapo asilimia 49 wanasema ubora wa elimu
umeongezeka na asilimia 36 wakibainisha kuwa elimu imezorota huku
asilimia 14 wakisema hakuna mabadiliko yeyote.
Utafiti huo umebainisha kuwa wazazi wengi walikuwa wanaelemewa na
michango ya shule ambapo wazazi na walezi 9 kati ya 10 huchangia elimu
katika shule za umma.
Asilimia 89 ya wazazi wanakiri kulipa michango shuleni na asilimia 80
wakiripoti kulipa mpaka Sh50000 kwa mwaka huku asilimia 8 wakilipa
zaidi ya Sh 100,000 kwa mwaka.
Utafiti huo pia umebainisha kuwa asilimia 37 ya wananchi wanaamini
kuna uhusiano wa karibu kati ya jitihada za mwalimu na matokeo ya darasa
la saba.
No comments:
Post a Comment