Halmashauri nchini zimeshauriwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili
ziweze kupata mapato ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya serikali za mitaa. Hayo
yamesemwa Oktoba 27, 2017 mjini Dodoma na wawakilishi wa idara
mbalimbali za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) wakati wa mkutano uliojumuisha wanachama wa Policy Forum
(PF) na maafisa wa OR-TAMISEMI.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kukutanisha wanachama wa PF na
maafisa wa idara za OR-TAMISEMI kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa
pamoja hasa katika sekta ambazo zinaweza kuleta mabadiliko katika ngazi
ya serikali za mitaa.
Mkutano huo ulitanguliwa na utambulisho wa pande zote mbili ambapo
upande wa PF, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa (LGWG),
Kellen Mngoya alitoa usuli kuhusiana na mtandao wa PF na kazi
zinazofanywa na vikundi kazi viwili ambavyo ni Kikundi Kazi cha Serikali
za Mitaa (LGWG) na Kikundi Kazi cha Bajeti (BWG). Utambulisho wa
OR-TAMISEMI ulitolewa na Sebastian Kitiku ambaye ni Mratibu wa Idara
TAMISEMI.
Kitiku alianza kwa kutoa utangulizi wa jinsi ambavyo OR-TAMISEMI
ilivyoalikwa kwenye mkutano wa wanachama wa PF wa robo mwaka
uliofanyika 2016 na kuomba wanachama wa PF kutumia maarifa na ujuzi wao
katika kurahisisha miongozo iliyoandaliwa na OR-TAMISEMI kwa ajili ya
matumizi katika ngazi za Serikali za Mitaa nchini.
Kitiku alipongeza juhudi zilizoonyeshwa na wanachama wa PF hasa wa
kikundi kazi cha LGWG kwa kuweza kurahisisha miongozo hiyo kuwa katika
lugha rahisi. Alitaja miongozo hiyo kuwa ni:
- Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini;
- Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Upimaji wa Mwaka na
- Mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa: Mwongozo wa Utekelezaji na Uendeshaji.
Wajumbe wa kikao hicho pia walipata nafasi ya kuweza kujadili
suala la Serikali Kuu kuchukua baadhi ya vyanzo vya mapato vilivyokuwa
vinakusanywa na Halmashauri. Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo Kitiku
alieleza kuwa Serikali Kuu iliamua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ikusanye kodi katika vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa kwa kuwa
ilionekana Halmashauri hazikuwa na mifumo madhubuti ya kukusanya mapato.
Hata hivyo alieleza kuwa zoezi hilo ni la majaribio tu na linafanywa
kwenye Halmashauri 30 ambazo ni kubwa ili kupima ufanisi katika
ukusanyaji wa mapato.
Kitiku alieleza kuwa kwa sasa Serikali ina mpango wa kuboresha
upelekaji wa fedha katika ngazi za Halmashauri. Mpango huo umeainishwa
vyema katika vitabu vilivyoandaliwa na OR-TAMISEMI na kuandikwa kwa
lugha rahisi na kikundi kazi cha PF na vitazinduliwa Oktoba 28, 2017
mjini Dodoma.
Wajumbe wa mkutano huo waliitimisha majadiliano kwa kukubaliana kuwa
bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya
PF na OR-TAMISEMI. Pia OR-TAMISEMI iliiomba PF iwapatie watumishi wake
mafunzo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ili waweze kutekeleza
vyema shughuli zao za usimamizi wa utekelezaji wa SDGs katika ngazi za
mikoa na mitaa.
Pia ilipendekezwa kuwa kikundi kazi cha LGWG kiwe kinashirikiana na
Idara ya Serikali za Mitaa ya OR-TAMISEMI hasa katika kazi zinazohusiana
na mafunzo kwa madiwani au uchambuzi wa sera mbalimbali zinazohusu
Serikali za Mitaa, hili lilikuwa pia ni pendekezo litakalohitajika
kuonekana kwenye Hati ya Makubaliano. Wajumbe walikubaliana pia kuwa
wakati kikundi kazi cha LGWG kikiwa kinatembelea Halmashauri kiwe
kinaenda na angalau afisa mmoja kutoka OR-TAMISEMI.