|
JOHN KALAGE MKURUGENZI MTENDAJI HAKI ELIMU |
Ndugu Wananchi; Itakumbukwa kwamba Februari 13, 2015 Sera Mpya ya Elimu
na Mafunzo ya Mwaka 2014 ilizinduliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete. Sera hii inaanza kutumika
Mwaka huu (2016) wa masomo.
Sera hii, imefuta na kubatilisha matumizi ya sera nyingine za elimu
zilizokuwa zikitumika kabla ya Mwaka 2015, zikiwamo Sera ya Elimu na
Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996), Sera ya Taifa
ya Elimu ya Juu (1999) na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
kwa ElimuMsingi (2007).
Lengo la Sera hii, linatajwa kuwa ni kushughulikia changamoto za
ki-elimu ambazo zinajitokeza zikiwemo udhaifu katika mfumo wa elimu na
mafunzo, uhaba wa walimu, uhaba wa zana, nyenzo na vifaa na miundombinu
ya kufundishia na kujifunzia pamoja na changamoto katika ithibati na
udhibiti wa ubora wa shule na vyuo katika ujumla wake ambavyo
vimechangia katika kushuka kwa ubora wa elimu na mafunzo nchini.
Ili kufanikisha lengo hilo, Sera imependekeza hatua mbalimbali ikiwamo
kupunguza miaka ya kupata elimu kutoka 18 (2+7+4+2+3+) hadi 16
(1+6+4+2+3); Kiswahili na Kiingereza kuwa lugha za kufundishia katika
ngazi zote, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kutoa
ElimuMsingi bila Ada sambamba na kupunguza michango ya wazazi shuleni.
Ndugu Wananchi; tukiwa miongoni mwa wadau muhimu katika kuhakikisha
maendeleo ya elimu nchini, HakiElimu kama shirika ambalo linataka kuona
elimu nchini ikiwa bora, yenye usawa na yenye kuwajengea uwezo wahitimu
kukabiliana na changamoto za kimaisha na ushindani katika soko,
tumepitia tumetathmini malengo na mapendekezo yaliyomo ndani ya Sera
hiyo, na tungependa kutoa maoni au msimamo wa shirika kuhusu Sera hii
mpya kama ifuatavyo:
Kuhusu ubora wa elimu
Pamoja na kuwa malengo ya sera yanataja kuhakikisha kuwa elimu
inayotolewa nchini inakuwa bora na ya viwango vya ushindani, sera
imeshindwa kufafanua ni jinsi gani itahakikisha kuwepo kwa ubora huo.
Katika uchambuzi tumeonesha kuwa tafiti nyingi zinakubali kuwa ili elimu
inayotolewa iwe yenye ubora ni lazima taifa lijitahidi kuboresha
mazingira ya ufundishaji na kuwekeza katika ubora wa walimu ambao ndio
msingi wa elimu yenyewe.
Hata hivyo Sera hii imekuwa kimya juu ya suala la ubora wa walimu na
mazingira yao ya kuishi na kufanyia kazi. Sera haitamki suala la
kuboresha maslahi ya mwalimu.
Aidha, ili kuhakikisha ubora mashuleni, shule, taasisi na vyuo vinapaswa
kufanyiwa ukaguzi kuhusu ufundishaji, ujifunzaji, mazingira n.k. Hata
hivyo sera hii haitoi mwongozo maalumu kuhusu namna ubora wa elimu
utakavyo tathiminiwa na jinsi ya kuimarisha ukaguzi. Itakumbukwa kuwa
Idara ya Ukaguzi kwa kipindi kirefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto
lukuki zikiwemo za uhaba wa bajeti na wataalamu. Takwimu zinaonesha kuwa
hali ya ukaguzi nchini hairidhishi kwani ni takribani 40% tu ya taasisi
za elimu ndizo hukaguliwa kwa mwaka..
Juu ya uwezo wa wahitimu kujiajiri,
Ndugu Wananchi lengo kubwa la mfumo wowote wa elimu duniani ni kuzalisha
rasilimali watu. Pamoja na Sera hii mpya kuzungumzia kwa ujumla kuwa
itaweka utaratibu utakaowawezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kushindana
katika soko la ajira pamoja na kujiajiri; haitoi mwongozo ni kwa namna
gani au hasa ni nini kitafanyika ili kuhakikisha lengo hilo
linafanikiwa.
Changamoto kubwa ya zao la rasilimali watu linalozalishwa na shule na
taasisi zetu imekuwa ni uwezo hafifu. Ushindani katika soko la ajira
umeiweka pembeni Tanzania kiasi kwamba katika kushindania kazi za
kimataifa tunashindwa kufua dafu hata mbele ya wenzetu wa Afrika
Mashariki mathalani kutoka Kenya, Uganda na hata Rwanda. Ripoti ya World
Economic Forum Network Readiness Index (2012 inaonesha kuwa Tanzania
inashika nafasi ya mwisho miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika
mashariki kwa kuwaandaa wananchi wake kuwa rasilimali watu yenye ujuzi
na maarifa bora. Sera kama mwongozo ilipaswa kutoa utaratibu wa jinsi ya
kulikabiri tatizo hili la uwezo wa wahitimu ili kuwezesha kuwa na
ujuzi na maarifa yatakayowafanya waweze kuajiriwa na kujiajiri kirahisi
zaidi.
Kuhusu lugha ya kufundishia
Ndugu Wananchi; Sera Mpya imeruhusu lugha za Kiswahili na Kiingereza
kutumika kama lugha za kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.
Tamko hili la kisera si tu ni ishara ya Taifa kutokuwa na msimamo juu ya
lugha ya kufundishia and kujifunzia, lakini pia sera haijabainisha
malengo mahsusi ya kutumia lugha mbili kufundishia katika ngazi zote za
elimu . Uchaguzi wa lugha ya kufundishia lazima ulenge kuwawezesha
wanafunzi kufundishwa na kujifunza ipasavyo ili kupata ujuzi na maarifa
tarajiwa. Pia uchaguzi wa lugha ya kufundishia lazima ulenge kuwawezesha
wahitimu wa kada mbalimbali za utaalamu kuweza kushindana katika soko
la kitaifa na kimataifa Tunaishauri serikali kutathmini utekelezaji wa
agizo hili la kutumia lugha mbili ikizingatiwa mambo mawili (a) urahisi
wa upatikanaji wa maarifa ya mjifunzaji yanayokidhi soko la ajira na
mwingiliano wa kijamii kati ya nchi na nchi.
Suala la usawa katika utoaji elimu,
Ndugu Wananchii; Pamoja na kuwa sera imetamka kuwa itahakikisha usawa
katika elimu inayotolewa, bado haikueleza ni kwa namna gani hilo
linaweza kufanikiwa wakati bado shule za umma zinakabiliwa na changamoto
nyingi za mazingira ya kujifunzia na kufundishia ukilinganisha na shule
binafsi.
Wakati wanafunzi katika shule za umma wakikosa walimu bora kutokana na
walimu kukimbia malipo duni na mazingira magumu, wakikosa vitabu na
maabara, wenzao katika shule binafsi wananufaika na mazingira mazuri,
hamasa ya walimu, uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na hivyo
kuwawezesha kufanya wafaulu vizuri katika masomo yao kuliko wanafuzni wa
shule za umma.
Kwa kushindwa kushughulikia suala hili, sera imeshindwa kupendekeza
mbinu za kuondoa matabaka ya kielimu nchini ambayo yanawagawa watoto wa
masikini kusoma kwenye shule zenye mazingira duni ya kufundishia na
kujifunzia na watoto wa wenye uwezo kusoma katika shule zenye mazingira
mazuri. Ikumbukwe kuwa wanafunzi walioko kwenye shule za umma ni
asilimia 94.7 ya wanafunzi wote walioko elimumsingi kwa takwimu za
mwaka wa 2015.
Rai yetu ni kuwa, ili kuleta usawa katika ujifunzaji ni lazima serikali
ikishirikiana na wadau wa elimu iboreshe mazingira ya kufundishia na
kujifunzia katika shule za umma. Sera itoe mwongozo juu ya viwango
maalumu vinavyohitajika kabla shule yeyote haijasajiliwa ili kuanza
kutoa huduma elimu kama inavyofanya kwenye shule binafsi. Ni vyema pia
viwango hivi vikahusisha kuwepo kwa miundombinu bora na ya kutosha
vikiwamo nyumba za walimu, madarasa, vyoo, maji, maktaba, maabara na
vifaa vyote muhimu vya kufundishia na kujifunzia.
Kuhusu ElimuMsingi bila Ada
Ndugu Wanahabari; Pamoja na kuwa wazo hili ni zuri na linaungwa mkono na
wadau mbalimbali wa elimu ikiwamo HakiElimu, sera haikutoa utaratibu
maalumu wa jinsi ambavyo tamko hili litafanikiwa. Serikali ni lazima
ikumbuke kuwa kuwaweka shuleni watoto na wakajifunza ipasavyo kunahitaji
gharama, tumeshuhudia utekelezaji wa sera ya elimu ya 1995 kupitia
miradi ya MMEM na MMES ikishindwa kutokana uhaba wa bajeti.
Tayari serikali imeanza kutekeleza mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa
kuondoa ada na michango. Japo serikali imedhamiria kutoa 100% ya fedha
za ruzuku kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa shule, bado kuna
changamoto ya namna gani serikali itasaidia uboreshaji wa miundombinu
shuleni ikizingatiwa kuwa shule hazipati fedha za shughuli za maendeleo
na zimekuwa zikitatua matatizo ya miundombinu kwa kutumia michango ya
wazazi. Tayari suala la elimu bila malipo limeanza kuleta mkanganyiko
kwa wazazi na walimu wakuu hasa kuhusu uchangiaji wa kuboresha
miundombinu ambao bado haujawekwa bayana na serikali. Serikali haina
budi kuandaa mkakati utakaowezesha utekelezaji wa elimu bila malipo huku
ikilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katia shule
zote za umma.
Ndugu Wanahabari; HakiElimu inapendekeza yafuatayo yawekwe kwenye
miongozo ya utekelezaji wa Sera hii ili iweze kuleta tija na kusaidia
kuboresha elimu yetu nchini.
Kama Taifa tunapaswa kutambua kuwa ulimwengu wa sasa wa sayansi na
teknolojia unazifanya nchi na mataifa kuhusiana kwa karibu zaidi kuliko
ilivyokuwa awali na hakuna taifa litakaloweza kuishi kama kisiwa. Ni
muhimu Tanzania ikafanya tathmini hii na kuweka bayana msimamo wake
kuhusu lugha tunayotaka kuitumia katika kuelimisha jamii na kizazi chetu
kijacho. HakiElimu inaona kuwa njia pekee ya kutatua suala hili ni
kuchagua lugha ambayo itaendana na uwekezaji ili kuwe na tija katika
ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi ili wanafunzi wapate maarifa na
ujuzi stahili na kuweza kushindana katika masoko ya ajira kimataifa
Suala la umri na miaka ya mwanafunzi kukaa shuleni lisipewe uzito kiasi
cha kusahau jukumu la msingi la elimu nchini ambalo ni kuelimisha na
kupandikiza weledi kwa watoto wetu. HakiElimu tunapendekeza badala ya
kuweka uzito katika umri wa mwanafunzi, ni vema ikaangalia zaidi nini
mwanafunzi anajifunza na vipi kinamsaidia katika kukabiliana na
changamoto za kimaisha.
Kwa kuwa Sera bado inaruhusu taasisi binafsi na wadau kushiriki katika
utoaji elimu nchini, ni muhimu pia ikaweka utaratibu maalumu wa jinsi
ambavyo shule za umma zitaboreshwa ili kuondoa tofauti ya shule za umma
na binafsi na hivyo kuondoa matabaka kielimu.
Ubora wa elimu umekuwa ni changamoto ya muda mrefu sasa na ni muda
muafaka kwa serikali kuandaa mikakati itakayowezesha kuboresha elimu
yetu katika ngazi zote za elimu. Njia pekee ya kufanikisha hili ni kuwa
na shule bora za umma ambazo zinahudumia wanafunzi wengi, kuwa na walimu
bora na wenye hamasa ya kufundisha, kuwa na mifumo ya kufuatilia na
kutathmini kiwango cha elimu katika ngazi zote na mifumo bora ya
usimamizi wa shule.
Mwisho tunaipongeza Serikali kwa juhudi za kuhakikisha Sera ya Elimu na
Mafunzo ya 2014 inapatikana.Hii ni baada ya kuwepo kilio cha muda mrefu
kutoka kwa umma na wadau wa elimu kudai kufanyiwa marekebisho kwa sera
za elimu za zamani ambazo ni dhahiri zilikwishapitwa na wakati na hivyo
kushindwa kukabiliana na changamoto mpya za elimu.
Imetolewa na Idara ya Habari na Utetezi
HakiElimu
Mawasiliano: media@hakielimu.org